Kitabu Cha Habakuki Mwandishi: Habakuki Mwaka: kati ya 612 -589 Kabla ya Kuzaliwa Kristo Wahusika wakuu: Habakuki na Wakaldayo Yaliyomo: 1. Swali la Habakuki na Jibu la Mungu, Sura 1:1—1:11 2. Swali la Pili la Habakuki na Jibu la Mungu Sura 1:12 – 2:20 3. Maombi ya Habakuki, Sura 3 Maana ya Jina Habakuki Habakuki, ambaye maana yake ni “kumbatia” au “mshindani mweleka”. Mwandishi wa kitabu hiki haelezi maisha yake binafsi na hataji kwa uwazi mwaka alipotoa ujumbe. Habakuki alikuwa nabii wa Yuda kutoka kabila ya Lawi. Alikuwa ni mmoja wa waimbaji wa hekaluni. Maudhui ya Kitabu hiki: Kitabu hiki kimeandikwa kwa mtindo wa mazungumzo kati ya Mung una nabii (Habakuki). Kitabu hiki kinazungumzia suala la mateso, dhambi na haki ya Mungu kama ilivyo kwa Ayubu na Zaburi ya 73. Nabii Habakuki katika Mazungumzo yake na Mungu, anaonyesha kushindwa kwake kuelewa ni kwa jinsi gani Mungu angeweza kuwatumia Wakaldayo, taifa ovu kuliko wayahudi (Israeli) kutekeleza hukumu ya Mungu juu ya taifa la Israeli, taifa lililokuwa limechaguliwa na Mungu. Habakuki anaanza kwa kumlalamikia Mungu kuwa Yuda hakutekeleza ujumbe aliopewa. Anauliza, hadi lini Yuda waendelee katika uovu bila kuadhibiwa. Mungu anajibu kuwa anaandaa adhabu itakayotolewa kwa kutumia Wakaldayo (Wababeli). Habakuki anabisha mpango huo akisema: kama Mungu ni Mtakatifu na wa haki, na Wayahudi ni watu wake itawezekanaje Wakaldayo wenye maovu mengi kuliko Wayahudi (Israeli) watumiwe na Mungu? Jibu la Mungu ni kuwa kila dhambi huleta hukumu. Hivyo wote watapata adhabu ya uovu wao. Mungu pia anamwambia Habakuki Mwenye haki ataishi kwa Imani, na Kwamba wanapaswa kuwa na uhakika ya kwamba Mungu alikuwa anafanya lililo sahihi kuwatumia wakaldayo walio waovu kutekeleza hukumu au adhabu yake kwa wana wa Israeli waliokuwa ni taifa teule. Pamoja na Hayo Mungu anamwambia Habakuki, Muda si mrefu wakldayo nao wangepata hukumu yao. Ujumbe Wa kitabu hiki: Ujumbe wa Habakuki ni BWANA Mungu sio Mungu wa Israeli na Yuda tu, yeye ni Mungu wa ulimwengu wote. Yuda na Kaldayo (Babeli) wataadhibiwa kwa kufuata maovu yao. Vile vile amtegemeaye Mungu akawa mwadilifu hana haja ya kuogopa hukumu maana “Mwenye haki ataishi kwa Imani”. Mungu atampa ushindi (2:4). Kusudi la Ujumbe wa Kitabu hiki Ni kuonyesha kwamba, Mungu ndiye nayeitawala dunia. Hata kama tunaona uovu na maovu yakiongezeka sana, Hata hivyo Mungu ataadhibu uovu na waovu siku moja na kuutowesha usiwepo tena. Wazo kuu la Kitabu hiki Mungu anaweza kutumia yeyote hata waovu kuadhibu watu wake walioitwa kwa jina lake wanapokwenda kinyume na maagizo yake; nia ikiwa ni kuwakumbusha na kuwarudisha watu wake katika njia sahihi. Hata hivyo, waovu hawa wakiisha kutimiza kusudi la Mungu nao huadhibiwa kwa uovu wao. Mambo Muhimu 1. Mungu hutumia waovu kuwaadhibu watu wake wanapokosea 2. Imani na Mamlaka ya Mungu yanatupa uhakika ya kwamba Mungu ana haki katika njia zake zote.