Habari zenu! SOMO LA TAREHE 6 Mei, 2021 Tazama maneno yaliyopo hapo chini na taja namna yanavyotumika. Du!, lo! ,jamani! Oyee!, yarabi!, ehe!, laa!, ayaa!, aka!, ala!, shabash!, ewaa!, aisee!,mmh!, balaa! Poa! Miamia!`, mamaa! Chubwi!, pa!, balaa! VIHISISHI Lengo: wanafunzi waweze kuelewa vihisishi, aina zake na namna ya kutumia katika mazungumzo/kuandika Ujuzi: Ustadi katika vihisishi Vihisishi ni maneno yanayodokeza vionjo au miguso ya moyo au ya akili. Vionjo vya moyo huweza kuwa vya furaha au huzuni. Maneno hayo kwa kawaida hupewa alama ya mshangao (!), au hutengwa kwa mkato (,) yatokeapo katika maandishi. Mifano ya maneno hayo ni loo!, ebu!, la asha! n.k. Kila kihisishi huweza kuibua hisia mahususi. Kwa hiyo ni vyema kutumia kihisishi kinachofaa. MAKUNDI YA VIHISISHI _huonesha hisia za ndani kama vile a)Mshangao b)Huzuni c)Furaha d)Majuto e)Huruma ama masikitiko Mifano ya Vihisishi 1. Lo! - hutumika kuonyesha mshangao, furaha, hofu au mshtuko na hali ya kubung'aa. 2. Masalale! - huonyesha mshangao 3. Do! au Du! - huonyesha mshangao; hali ya kutoamini. 4. Salaala! - huonyesha mshangao wa hali ya juu. 5. Ebo! - huonyesha mshangao; hali ya dharau na kutoamini. 6. Aka! - huonyesha mshangao; hali ya kukanusha jambo. 7. Ah! - huonyesha hali ya kukereka. 8. Ahaa! - huonyesha furaha; uchungu;kukubali;kukataa. 9. Aa! - huitikia; kukubali; kukataa; hali ya kuchanganyikiwa. 10. Po! - huonyesha dharau. 11. Pukachaka! - huonyesha kukidharau kitu; kutokithamini kabisa. 12. Oyee! - huonyesha furaha, shangwe na hali ya kupongeza. 13. Yarabi masikini! - hushangaa na kuomba msaada kwa mwenyezi Mungu. 14. Ewaa! - huonyesha kuitisha kuwa mambo ni sawa. 15. Hewaa! - hukubali kuwa mambo ni sawasawa;barabara! 16. Taib! - hukubali kuwa ni vyema au vizuri. 17. Shabash! - huonyesha furaha au mshangao 18. Ala! - huonyesha mshangao au mshtuko. 19. Aisee! - humfanya mtu asikilize unayotaka kumwambia; ohaa! abaa! 20. Cho! - huonyesha mshangao; lo! cha! 21. Chup! - humwambia mtu anyamaze kwa hasiraau dharau; kimya! chub! 22. Us! - humnyamazisha mtu kwa hasira au dharau. 23. Ehee! - huonyesha ukubaliano au hamu ya kuendelea kusikiliza; ehee! 24. Epuu! - huonyesha kutompa mtu hima ya kufanya au kutamka alilonuia; kutoamini analotamka. 25. Ewe! - huonyesha mshangao na mgutuko. 26. He! - huashiria wito wa kuhadharisha. 27. Aa-aa! - hunyamazisha, huzomea au kukemea. 28. Oh! - huonyesha mshangao; kutoamini yaliyosemwa. 29. Oofuu! - huonyesha uchovu au kuvuta pumzi kwa uchovu. 30. Mmh! - hali ya kutoamini unaloambiwa. 31. Afanalek! - huonyesha kupigwa na butwaa, kushtuka. 32. Audhubillahi! - huonyesha mshangao na kumlaani shetani. 33. Mnh! huashiria kuitikia kwa wasiwasi, hofu na mshangao. 34. Hee! - huonyesha mshtuko wa kutahadharisha au kuonya. 35. Ohoo! - hukashifu. 36. Zii! - hukemea; hulaani; kinyume cha kushangilia. 37. Yarabi Stara! - huashiria kuomba ulinzi kwa Mwenyezi Mungu. Zoezi Tunga sentensi mbili kwa kuonesha hisia za: a)Kukereka b)Kupongeza c)Kuhimiza d)Kunyamazisha e)kusikitisha